Share news tips with us here at Hivisasa

Mwanasiasa aliyewania kiti cha ubunge katika eneo bunge la Kitutu Chache kaskazini kaunti ya Kisii, James Atandi ameomba serikali ya kaunti ya Kisii kutoajiri watu kwa msingi wa kiukoo na kuajiri watu wote bila kupendelea watu wengine.

Akizungumza siku ya Ijumaa katika hafla ya mazishi ya Monyeche Nyakundi yaliyoandaliwa katika uwanja wa shule ya Upili ya wavulana ya Nyakeiri, iliyoko katika eneo bunge hilo, mwanasiasa huyo alidai kuwa serikali ya kaunti ya Kisii imekuwa ikiwaajiri watu kwa msingi wa kiukoo.

Alisema sharti uwazi uonyeshwe kwa watu wote wa kaunti hiyo.

“Waliowachagua viongonzi ni wapiga kura katika kaunti ya Kisii. Wakati watu wanapoajiriwa, sharti watu wote kila sehemu ya kaunti hii wapate kazi. Ni makosa kwa serikali kupendelea watu fulani na kuwasahau wengine," alisema Atandi.

Mwanasiasa huyo pia alisema kuwa kama angechaguliwa kuwa mbunge wa eneo bunge hilo la Kitutu Chache kaskazini mwaka wa 2013 angebadilisha shule ya upili ya wavulana ya Nyakeiri kuwa na sura mpya ikilinganishwa na jinsi ilivyo kwa sasa.

Shule hiyo imekuwa na upungufu wa wanafunzi ikilinganishwa na jinsi ilivyokuwa hapo mbeleni.

Kwa sasa shule hiyo ina wanafunzi chini ya 200 jambo ambalo halifurahishi wakaazi wa eneo hilo.

“Mwaka wa 2017 nitakiwania kiti cha ubunge katika eneo hili. Nawahitaji mnichague ili nibadilishe shule zote za eneo hili iziwe na sura mpya. Mnaona matokeo ya viongozi muliowachagua jinsi yalivyo,” alisema Atandi.

Wakaazi wa eneo hilo waliokuwa kwa hafla hiyo ya mazishi walisema kuwa Atandi ameongea ukweli wa mambo haswa kuhusu uajiri wa watu katika kaunti ya Kisii.