Licha ya vijana wengi kujitahidi kunufaika na kandarasi zinazotolewa na Serikali ya kaunti ya Mombasa, vijana hao kamwe hawajapewa nafasi hizo.
Akizungumza mjini Mombasa siku ya Jumamosi, Mkurugenzi wa Shirika la kijami la Kenya Community Support Centre eneo la Pwani Phyllis Muema alisema ubaguzi kama huo ndio uliyowapelekea vijana wengi kujiunga na makundi ya kihalifu na yale ya kigaidi, na ni lazima serikali ya kaunti hiyo iwathamini vijana.
Muema alisema katiba imeweka wazi kwamba asilimia 30 ya zabuni zinazotolewa na serikali za kaunti zinapaswa kuwaendea vijana, wanawake na walemavu katika kaunti hiyo lakini zabuni hizo zimewanufaisha mabwenyenye pekee.
“Tunasikitika kuona kwamba zabuni zinazotolewa na serikali ya kaunti yetu hazijawafaidi vijana wala wanawake kutokana na zabuni hizo kutolewa kwa ubakuzi," alisema Muema.
Mwanaharakati huyo wa kijamii anaitaka serikali ya kaunti ya Mombasa kuhakikisha inazingatia sheria hiyo ili kuinua hali ya maisha ya jamii mashinani hususan wanawake, vijana na walemavu.
Mapendekezo yake yanajiri baada ya wakazi wa kaunti hiyo kulalamikia ubaguzi mkubwa wa ugavi wa zabuni ili kuwawezesha wakazi kufanikisha kandarasi na kujikimu kimaisha.
Maelezo ya picha:
Mkurugenzi wa Shirika la kijami la ‘Kenya Community Support Centre’hapa Pwani Phyllis Muema.Alisema kwamba ubaguzi umechangia vijana wengi kutoza zabuni kutoka kwa kaunti ya Mombasa.