Mwakilishi wa Wadi ya Kisii Central, Bw Wilfred Monyenye ameitaka serikali ya Kaunti ya Kisii kuwashirikisha wakazi kwa upandaji miti na maua.
Mwakilishi huyo aliwataka maafisa wakuu pamoja na idara ya mipangilio ya kaunti kuangalia suala la upandaji maua na miti kama njia mojawapo ya kutunza mazingira.
Pia alipendekeza uwepo wa maafisa maalumu wa kusimamia usafi wa mji huo na kuwadhibiti baadhi ya watu ambao wamekuwa wakikata miti na kuchafua barabara za mji huo.
Mwakilishi Monyenye aliyekuwa akitoa hoja katika Bunge la Kaunti hiyo alisisitiza kuwa mji wa Kisii sharti uwe kivutio cha watalii kwa kupitia ushirikiano wa pamoja baina ya wakazi na serikali ya hiyo.
Aidha, aliweka wazi kuwa atajitahidi vilivyo kuboresha mji yeye kama mwakilishi wa wadi kwa ushirikiano na serikali ya kaunti.
Mji wa Kisii umeshuhudia kukatwa kwa miti sio tu na wakazi, bali shirika la kusambaza nguvu za umeme nchini (Kenya Power) ambalo limekuwa likipunguza kwa kukata baadhi ya miti ambazo zimepitisha matawi yake kwenye nyaya za umeme na zile miti ambazo zimepandwa karibu na vikingi vya umeme ili kuepusha na hatari ya nguvu za umeme kusababisha maafa.
Monyenye amesema haya siku moja kabla ya kukamilika kwa kongamano la kujadili uhifadhi na udhibiti wa vifaa vya kielektroniki na umuhimu wa kuweka mazingira salama lililoendelea kwa siku tatu na kufika kikomo jana Alhamisi.