Mwakilishi wa wadi katika bunge la Kaunti ya Nakuru, ametoa changamoto kwa serikali hiyo kujenga vituo vya kurekebishia tabia angalau kwa kila eneo bunge, kwa manufaa ya waliokuwa waraibu wa pombe haramu na dawa za kulevya.
Akizungumza siku ya Ijumaa katika mkutano na kikundi cha Bahabiri, kwenye ukumbi wa Kanisa la PCEA Ngwataniro Bahati, kilichobuniwa miezi miwili iliyopita na akina mama waliokuwa waraibu wa pombe, mwakilishi wa wadi ya Bahati, Peter Nderitu, alisema hilo linawezekana kwa ushirikiano wa serikali kuu na ya kaunti, baada ya oparesheni ya kumwaga pombe kufanikiwa pakubwa.
Nderitu alimfananisha Rais Uhuru Kenyatta na Musa aliyewatoa utumwani wana wa Israeli, kutokana na jinsi ameokoa kizazi cha sasa kutoka kwa mauti ya pombe haramu.
“Pahali tulikuwa ni katika utumwa kama wana wa Israeli. Hatungekosa kuskia maafa yaliyotokana na pombe haramu kila siku lakini Mungu ni mwema tulipata Musa wa kututoa huko,” alisema Nderitu.
Aliongezea: “Huko Murang’a na Kiambu wameweka vituo vya kurekebisha tabia. Ni bora kaunti yetu ikiiga mfano huo na kujenga kituo kimoja angalau kwa kila kaunti ndogo.”
Kikundi cha Bahabiri sasa kimevutia sio tu waliokuwa wamekwama kwenye ulevi, mbali pia wazee, vijana, wanabiashara na watu wa kanisa na hukutana mara moja kwa mwezi huku idadi yake ikiongezeka kutoka 63 hadi 130 katika muda wa miezi miwili tu.