Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Serikali ya kaunti ya Kisii imeombwa kukarabati uwanja wa michezo ulioko katika wilaya ya Marani eneo bunge la Kitutu Chache kaskazini kaunti ya Kisii ili kuwa wa hali ya kisasa jinsi ilivyoahidi hapo mbeleni.

Hii ni baada ya uwanja huo kuharibika, ilhali unatumiwa kila wikendi na vijana wakati wa vinyanganyiro mbalimbali ambavyo huandaliwa na wanasiasa pamoja na wahisani wengine.

Akiongea na waandishi wa habari siku ya Jumanne katika uwanja huo ulioko karibu na shule ya wasichana ya Marani, msimamizi wa uwanja huo ambaye pia anasimamia kandanda katika wilaya hiyo Peterson Osante aliomba serikali ya kaunti kuukarabati uwanja huo ili uendelee kutumiwa.

“Naomba serikali ya kaunti itukarabatie uwanja huu maana ni wa willaya ya Marani ambayo inastahili kuwa na uwanja mzuri,” alisema Osante.

Ikumbukwe kuwa viongonzi mbalimbali ambao wamewahi kuwa wabunge katika eneo bunge hilo la Kitutu Chache walikuwa wakiahidi uwanja huo kukarabatiwa, jambo ambalo halijazaa matunda hadi sasa.

Mmoja wa viongonzi ambao waliahidi kukarabati uwanja huo ni mbunge Richard Onyonga, ambaye aliwahi kuwa mbunge katika eneo hilo na baadaye eneo bunge hilo likagawa mara mbili na kuwa Kitutu Chache Kusini na kaskazini, huku mbunge katika eneo hilo ambapo uwanja huo uliko ni Jimmy Angwenyi, ambaye hajawai kuzungumzia ukarabati wake.