Mbunge wa eneo bunge la Kitutu Masaba, Kaunti ya Nyamira Timothy Bosire ameiomba serikali ya Kaunti ya Nyamira kuhakikisha sekta ya afya, elimu na ile ya uchukuzi zimeshughulikiwa kikamilifu.
Akizungumza siku ya Jumapili katika shule ya msingi ya Kebirigichi alipokuwa akitembelea miradi yake mbalimbali ya maendeleo, mbunge huyo alisema ikiwa serikali ya kaunti inataka wananchi wa kaunti hiyo kufurahia uongonzi ulioko, sharti ifanye maendeleo.
Aidha, mbunge huyo aliomba serikali ya kaunti hiyo kuhakikisha wananchi wamekarabatiwa barabara zote na vyuo vya ufundi vimejengwa vizuri ili wanafunzi waweze kupata mafunzo ya kiufundi ili waje kujisaidia nyakati zijazo.
Aliongezea kuwa serikali ya kaunti inapaswa kuimarisha sekta ya afya kikamilifu kwa kununua madawa ya kutosha katika hospitali zote za kaunti hiyo.
“Naomba serikali ya kaunti kufanya yale inastahili kufanya kwa wananchi wa kaunti hii. Sekta ya elimu ipewe kipau mbele pamoja na ile ya afya maana bila hizo mbili hatutaenda popote,” alisema Bosire.
Wakati huo huo, mbunge huyo aliahidi kujenga mijengo mipya ambayo ni ya kisasa katika shule ya msingi ya Kebirigichi kwani mijengo ilioko kwa sasa ni ya zamani sana.
Alisema kupitia hazina ya ustawi ya maeneo bunge, atajenga mijengo hiyo ili wanafunzi nao waweze kusomea mahala palipo na mazingira mema ambayo ni ya kupendeza na ya kufurahisha kama njia mojawapo ya kuwatia motisha wanafunzi kusoma kwa bidii.