Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Mbunge wa eneo bunge la Bobasi kaunti ya Kisii Steve Manoti ameiomba serikali ya kaunti ya Kisii kutumia pesa walizokabidhiwa kutoka serikali kuu kufanya maendeleo katika kaunti nzima ya kisii vizuri.

Akizungumza siku ya Jumapili katika hafla ya mazishi ya Benson Onchweri Nyakenyanya, yaliyoandaliwa katika wadi ya Nyamasabi ilioko eneo bunge la Nyaribari Masaba, mbunge Manoti alisema sekta ya afya na ile ya maji ziliwekwa chini ya serikali za ugatuzi na kuomba serikali ya Kisii kuinua sekta hizo kikamilifu.

Manoti aliomba serikali ya kaunti hiyo kujaribu iwezavyo kuhakikisha wananchi wamefanyiwa maendeleo kikamilifu.

“Sisi wabunge kutoka kaunti ya Kisii tuliunga mkono serikali ya kaunti yetu na sharti maendeleo yafanywe kikamilifu,” alisema  Manoti.

Aliongeza: "Naomba kazi ionekane kwa wananchi kuanzia wadi mbalimbali hadi kwa maeneo bunge ili sisi sote tuweze kuridhika na kusema kuwa serikali ya kaunti yetu imefanya maendeleo.”

Matamshi ya mbunge Manoti yaliungwa mkono na mbunge wa Nyaribari Masaba Elijah Moindi ambaye alisema watafurahi wakiona serikali ya kaunti ikifanya maendeo zaidi haswa katika sekta ya afya na kutumia pesa vizuri bila tashwishi yoyote.

“Hapo mbeleni, sisi wabunge ndio tuliokuwa tukijenga hospitali na kununua dawa lakini kwa sasa serikali za kaunti ndizo zlizochukua jukumu hilo. Sasa kazi yetu ni kutembelea hospitali kuona yale ambayo serikli ya ugatuzi imefanya,” alisema Elijah Moindi.