Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Serikali ya kaunti ya Mombasa imepinga madai ya kupokea mlungula katika kutoa zabuni kwa vijana na wafanyibiashara katika kaunti hiyo.

Kulingana na Mwenyekiti wa Kamati ya Uchukuzi na Miundo Msingi katika bunge la kaunti hiyo Amir Thoya, viongozi wa kaunti hiyo hawajashiriki kashfa zozote za kupokea hongo kutoka kwa wakazi ili kuwapa zabuni.

Akiongea mjini Mombasa siku ya Alhamisi, Thoya alisema kwamba viongozi wa kaunti hiyo wanafwatilia kwa karibu mno shughuli za utoaji zabuni na endapo afisa yoyote atapatikana akipokea hongo ili kutoa zabuni za kaunti, atachukuliwa hatua kali za kisheria.

“Sisi kama kamati ya uchukuzi na miundo msingi hatujawahitoa zabuzi kwa vijana wala wafanyibiashara kwa kupewa hongo na hatuwezi kubali jambo hilo kutekelezwa katika afisi za kaunti hii. Yeyote atakepatika mkono wa sheria utamandama,” alisema Thoya.

Wakati huo huo, Thoya aliwahimiza vijana, akina mama na watu wanaoishi na ulemavu kujitokeza na stakabadhi hitajika za usajili kutoka kwa idara za serikali na kujaza fomu za kupata zabuni hizo ili kujiendeleza kimaisha.

“Tunawaomba vijana, akina mama na jamii ya watu wanaoishi na ulemavu kujitokeza na stabadhi hitajika za usajili wa zabuni na sisi kama kaunti, tutawapa zabuni hizo ili nao waweze kufanya miradi mbalimbali ya kuwakimu kimaisha.

Hatua hiyo imejiri baada ya tetesi kuzuka kuwa baadhi ya maafisa wa serikali ya kaunti ya Mombasa huitisha hongo kabla ya kutoa zabuni na kandarasi kwa wakazi.