Serikali ya kaunti ya Kisii imepongezwa kuwa kukarabati baadhi ya barabara katika wadi mbalimabli za kaunti hiyo kama njia moja ya kuinua viwango vya uchukuzi katika kaunti hiyo.
Wakiongea siku ya Jumanne katika sehemu ya Omosocho wadi ya Kisii ya Kati eneo bunge la Nyaribari Masaba, baadhi ya wakazi walipongeza serikali ya kaunti ya Kisii kwa kukarabati baadhi ya barabara katika wadi hiyo haswa barabara ya Omosocho-Itibonge-Menyinkwa.
Wakazi hao wanaotumia barabara hiyo wamepongeza serikali ya kaunti ya Kisii kwa kuwakumbuka kwa kuwa barabara hiyo imekuwa ikiwasumbua hasa wakati mvua nyingi inaponyesha katika eneo la Kisii.
“Nimatumaini yangu kuwa barabara hii ikikamilika kukarabatiwa shida ya kusumbuliwa na matope hasa wakati wa mvua itaisha na biashara itanawiri katika eneo hili," alsema Reuben Mosiria, mkazi.
Wamiliki wa nyumba katika eneo hilo walisema kuwa wao hukosa wateja kwa ukosefu wa barabara lakini wamefurahishwa na juhudi za serikali kuanza kukarabati barabara hiyo.
“Wateja wengi hukataa kukodisha nyumba katika eneo hili kwasababu ya hali mbaya ya barabara lakini sasa nitapata wateja wengi kwa vile serikali ya kaunti imeanza ukarabati wa barabara hiyo,” alisema Rosyline Mocheche, mmiliki wa nyumba katika eneo hilo.
Aidha, wamepongeza mwakilishi wa wadi hiyo ya Kisii ya Kati Fred Monyenye kwa kazi anayofanya ya kuhakikisha kuwa wakazi wananufaika na matunda ya serikali za ugatuzi haswa kwa kukarabatiwa barabara katika wadi hiyo.