Waziri wa ardhi na mipangilio ya mji katika kaunti ya Mombasa Francis Thoya amesema kuwa ataendelea kufungua njia na kukarabati mabomba ya kupitisha maji, na kubomoa majengo ambayo yameziba njia.
Aidha, ameongezea kuwa kaunti hiyo inafanya hili ili kuepusha madhara na athari ambazo huenda zikachangiwa na mvua nyingi ya El Nino ambayo tayari imeanza kunyesha tangu juzi.
Bwana Thoya aidha amesema kuwa watakuwa wanabomoa majengo pamoja na nyumba ambazo zimejengwa maeneo hayo kinyume na utaratibu wa usanifu-majengo.
Akiongea na wanahabari mjini Mombasa siku ya Jumatano wakati wizara yake ilikuwa katika harakati za kuyabomoa majengo ambayo yamejengwa bila utaratibu, waziri huyo alisema kuwa yupo tayari kukabili mvua hiyo ya El Nino ambayo imeanza kuonyesha dalili ya kunyesha kwa wingi.
Aliwataka wakazi kushirikiana na wizara yake kwa kutoa ripoti ya dharura na kutilia maanani taarifa kutoka katika idara ya hali ya anga ambayo imewataka wakazi kutafuta mahali salama iwapo wataathirika na mvua hiyo.
Tayari idara ya hali ya anga imetoa tahadhari kwa wakazi kuwa makini huku mvua hiyo ikinyesha zaidi siku ya Jumanne na siku ya Jumatano.
Baadhi ya wakazi wameitaka serikali kuu kuwaelekeza ni wapi wanahitajika kuzuia dhidi ya mvua hiyo badala ya kuendelea kuwaambia kuwa watorokee maeneo ya juu kila mara.