Mwenyekiti wa magari yanayohudumu kwenye mji wa Kisii kuenda Nyamira ameiomba serikali ya kaunti kuchunguza na kudhibiti baadhi ya magari ambayo yana nambari za usajili za kigeni.
Akizungumza siku ya Jumapili, Bwana James Mosota alidai kuwa magari hayo yamekuwa yakisababisha ajali na kutoweka.
Haya yanajiri baada ya gari lenye usajili wa nambari ya Uganda kugonga matatu aina ya Nissan kwa upande wa nyuma wakati matatu hiyo ilikuwa imeegeshwa ili kupandisha abiria.
Mosota alisema kuwa baadhi ya magari ambayo yana nambari za usajili hasa za nchi ya Tanzania na Uganda yamekuwa yakipitia barabara hiyo kwa muda sasa, na visa takribani vitatu vimeshuhudiwa dhidi ya magari hayo.
Alidai kuwa magari hayo hugonga magari mengine ya abiria pamoja na wahudumu wa bodaboda na baadaye kutoweka na hakuna hatua ya kisheria huchukuliwa ili kuwashika na kuwashtaki wahusika.
Mosota alidai kuwa jambo hilo husababishwa na ukosefu wa maafisa wa trafiki kupiga udhibiti kwenye barabara hiyo.
Mwenyekiti huyo pia ameitaka idara ya polisi pamoja na serikali ya kaunti ya Kisii, kuhakikisha kuwa maafisa wa trafiki wanashika doria katika barabara hiyo ya Jogoo inayounganisha mji wa Kisii na Nyamira.
Aidha, Mosota aliisihi serikali ya kaunti kupitia wizara ya barabara na ujenzi kushawishi serikali kuu kukarabati barabara hiyo kwa kuweka matuta na kuziba mashimo ambayo alisema kuwa yamekuwa chanzo kikuu cha kuwepo kwa mikasa na visa vya ajali ambavyo huweza kuepukwa.