Share news tips with us here at Hivisasa

Mbunge wa eneo bunge la Kitutu Masaba, Kaunti ya Nyamira Timothy Bosire, ameiomba serikali kuchunguza mitambo ya transfoma ambayo inaendelea kuwekwa katika sehemu mbalimbali za mashinani.

Wito huo umetolewa baada ya kubainika kuwa mitambo ambayo huwekwa katika sehemu mbalimbali za mashinani si halali na huwa ghushi kwani huzimika kila wakati na kusababisha wananchi kukosa nguvu za umeme.

Kulingana na mbunge huyo, wanakandarasi wale ambao wanauzia kampuni ya umeme mitambo hiyo wanatakiwa kueleza ni wapi wanatoa mitambo hiyo ili ukweli ubainike.

Akizungumza siku ya Jumatatu katika eneo bunge lake, Bosire alisema wananchi wa sehemu za mashinani hukosa nguvu za umeme kila wakati kufuatia kukatika kwa nguvu hizo jambo ambalo lilimpelekea kusema mitambo ambayo inawekwa mashinani haina ubora, na kuhitaji serikali kuchunguza mitambo hiyo hutoka wapi.

“Mitambo ambayo hununuliwa na kuwekwa katika sehemu za mashnani iko katika samburi ya chini na haina ubora wowote ikilinganishwa na ile huwekwa mijini na husababisha nguvu za umeme kupotea kila wakati,” alisema Bosire.

Aliongeza: “Naomba serikali kujali maslahi ya watu kwa kuchunguza mitambo hiyo hutoka wapi ili ukweli ubainke. Tunahitaji pesa za serikali zitumike vizuri kwa kununua mitambo ambayo ni halali na iko na ubora wa juu.”