Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Wakulima wa nafaka kutoka North Rift wameitaka serikali kuwatengea fedha za kukausha mahindi wakati wa msimu wa El Nino unaotarajiwa kote nchini.

Wakulima hao wameelezea wasiwasi ya kupata hasara kubwa iwapo msimu wa El Nino utaendelea hadi mwezi wa kumi ikizingatiwa kuwa huo ndio wakati wa kuanza kuvuna mahindi na ngano.

Wakizungumza siku ya Jumatano, wakulima hao kupitia kwa mkurugenzi mkuu wa shirikisho la wakulima KFA Bw Kipkorir Menjo, wameitaka serikali kutoa fedha za ziada kwa bodi ya nafaka na mazao nchini NCPB ili kuwezesha bodi hiyo kutoa huduma za kukausha mahindi kwa wakulima kwa bei nafuu.

"Ni bayana kwamba tutalazimika kuvuna mahindi yetu mapema ili kukwepa hasara kutokana na El Nino. Serikali inapaswa kudhamini bodi ya NCPB ili kupunguzia wakulima gharama ya kukausha mahindi," alisema Bw Menjo.

Wakulima wengi kwa sasa wanajiandaa kuvuna mahindi yao mapema kutokana na hofu ya kupata hasara wakati wa msimu wa mvua ya El Nino.

Wakulima hao walisema hali hiyo itasababisha mahindi yao kuwa na unyevunyevu mwingi hivyo basi hawatapata faida inayostahili kwani dhamana ya mahindi yao itakuwa chini.

"Kwavile tutalazimika kuvuna mahindi yetu mapema, itakuwa jambo la busara kwa serikali kutoa kwa NCPB fedha zaidi ili kugharamia huduma ya kukausha mahindi ili wakulima wasipunjwe zaidi," alisema Bw Joseph Chumo ambaye ni mkulima.