Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Wakaazi wa lokesheni ya Mwomonari eneo bunge la Kitutu Chache Kaskazini kaunti ya kisii wameomba serikali ya kaunti ya kisii kufungua zahanati iliyofungwa hapo mbeleni katika eneo la Nyakeiri kufuatia ukosefu wa dawa.

 Wakiongea na mwandishi huyu wa habari siku ya Jumatatu katika eneo la Nyakeiri wakaazi hao wakiongozwa na George Osiemo waliomba serikali kufungua zahanati hiyo ili wakaazi wa eneo hilo waweze kupata matibabu karibu nao.

“Wakaazi wengi wa eneo hili hutembea kwa muda mrefu mpaka sehemu ya Marani na wengine huenda eneo la Nyagoto kutafuta matibabu. Tunaomba serikali ya kaunti ya kisii kufungua zahanati hii iliyoko karibu na sisi ili kutupunguzia mzigo wa kutembea safari ndefu,” alisema Hesbon Ombae, mkaazi.

Aidha, wakaazi hao walisema kuwa wao hutumia pesa nyingi kuenda hadi hospitali zingine badala ya kuhudumiwa karibu nao.

“Mke wangu alikuwa mgonjwa siku ya Ijumaa usiku wa manane nikashindwa cha kufanya. Ilibidi nimwite mwendeshaji pikipiki aje kupeleka mke wangu hospitalini. Baada ya kunifikisha katika Hospitali ya Marani aliniitisha shilling 400 badala ya shilling 100," alisema Haron Ochako, mkaazi.

“Kama serikali inataka sisi wananchi wa kawaida tufaidike, itawalazimu kufungua zahanati hii ya Nyakeiri ili nasi tufurahie uongonzi wa ugatuzi,” alidokeza George Osiemo.

“Ni jukumu la uongonzi wa serikali ya kaunti ya kisii kuelewa na kusikia kilio cha wakaazi hawa na kufungua zahanati hii," aliongeza Osiemo.