Share news tips with us here at Hivisasa

Huku vita dhidi ya dawa za kulevya katika eneo la pwani ukiendelea kushika kasi, mwakilishi wa wadi ya Shika Adabu, Bwana Mohammed Madundo, ameitaka serikali kuwapa usalama wale wakazi ambao wamekuwa wakiwaripoti wauzaji wa dawa za kulevya.

Hii ni baada ya kufuatia ripoti kuwa baadhi yao wamekuwa wakitishiwa maisha iwapo wataendelea kutoa ripoti kama hizo kwa polisi.

Akiongea siku ya Ijumaa wakati wa maandamano ya amani na wakazi wa Shika Adabu, kwenye harakati za kupinga matumizi na uuzaji wa dawa za kulevya kwa vijana na wakazi kwa jumla, Bwana Mohammed alisema kuwa wauzaji dawa hizo wamekuwa wakiwapa vitisho baadhi ya wanaharakati, pamoja na wakazi ambao wamekuwa katika mstari wa mbele kupigana dhidi ya uuzaji wa mihadarati.

Mwakilishi huyo alisema kuwa hali hiyo imeanza kuwatia hofu wakazi.

Aliitaka serikali kuu kwa ushirikiano na maafisa wa polisi ambao hupigana dhidi ya mihadarati, kuwahakikishia usamala wakazi na wanaharakati ili wawe na ujasiri wa kuendeleza kampeni hiyo, ya kuangamiza jinamizi hilo, ambalo alitaja kuwa kikwazo kwa maendeleo na masomo miongoni mwa vijana kutoka eneo pana la Pwani.

Hata hivyo, mkazi mmoja ambaye hakutaka kutajwa jina kwa sababu za kiusalama, alidai kuwa baadhi ya wauzaji wa dawa za kulevya kwenye kaunti ya Mombasa na Kwale wamekuwa wakifunikwa na maafisa wakuu wa polisi pamoja na baadhi ya viongozi.

Kamishna wa polisi kwenye kaunti ya Mombasa kwa upande wake aliwahakikishia wananchi kuwa usalama wao utashughulikiwa na kuwataka kuendelea kutoa ripoti dhidi ya yeyote ambaye wanamshuku kuwa anauza dawa za kulevya.