Mwenyekiti wa vijana wa kukwangura kokoto katika eneo la Nyambera, kaunti ya Kisii Gilbert Ongwae ameomba serikali ya kaunti kuwatafutia vijana hao kazi tofauti kwa kuhofya maisha yao katika eneo hilo.
Hii ni baada ya kijana mmoja wa umri wa makamo kupoteza maisha yake kwa kuangukiwa na mawe katika eneo hilo lililoko kilomita moja kutoka mji wa Kisii, alipokuwa akichimba migodi siku ya Jumatano, jambo lililowaacha wengine na mshtuko, na kuhofia maisha yao kwani wengi hutegemea migodi hiyo kupata riziki yao ya kila siku.
Akizungumza na waandishi wa habari siku ya Alhamisi, mwenyekiti huyo alisema hawana mahala pengine wanaweza pata riziki, na kuomba serikali ya kaunti kuwasaidia kuwatafutia kazi nyingine ya kufanya.
“Wengi wetu tumeoa na tuko na watoto na tumekuwa tukilisha familia kutoka eneo hili, lakini jinsi vijana wenzetu wameanza kupoteza maisha yao, ata sisi tumehofia sana,” alisema Ongwae.
“Hii si mara ya kwanza maafa ya aina hii kufanyika katika eneo hili, huyu ni wa tatu sasa tangu tuanze kufanya kazi ya kukwangura kokoto kwa takribani miaka 25 sasa iliyopita, tunaomba serikali yetu ya kaunti itusaidie ili nasi tuendelee na maisha,” aliongezea.