Wanabiashara wa kuuza mboga katika mji wa Nyamira wameomba serikali ya kaunti kuwatafutia soko ya kuuza mboga zao ili kukuza na kujiendeleza kibiashara.
Wakizungumza na mwandishi huyu mnamo siku ya Jumanne katika mji wa Nyamira, wanabiashara hao wakiongozwa na Jackline Bosibori walisema serikali ikiwatafutia soko haswa katika nchi za kimataifa watajikuza zaidi kibiashara.
“Tunaomba serikali ya kaunti ya Nyamira kututafutia soko ya kuuza mboga maana hapo mbeleni serikali hii ilituahidi tukipanda mboga kwa wingi watatutafutia soko ili tukuze biashara zetu, jambo ambalo tuliweza kulifanya kwa motisha,” alihoji Jeruza Momanyi, mwanabiashara.
Wakati huo huo, wanabiashara hao walisema wako tayari kupanda mboga kwa wingi ikiwa serikali itawajali kwa kuwatafutia soko hiyo
“Wengi wetu hutegemea uuzaji huu wa mboga maana tunawasomesha watoto wetu kupitia biashara hii, na tunaomba serikali kuungana nasi ili tujikimu zaidi kimaisha kwa kukuza biashara zetu,” alisema Rebeccah Onsano, mwanabiashara mwingine.
Sasa ni jukumu la serikali ya kaunti ya Nyamira kusikia kilio cha wanabiashara hao kwa kuwatafutia soko ya kimataifa ili kujiendeleza
Ikumbukwe kuwa saerikali ya kaunti hiyo iliwapa makundi ya akina mama hao mbegu ya mboga na kuwaahidi kuwa wanapovuna watawatafutia soko, jambo ambalo kwa sasa limeonekana kutimia kupitia kwa wanabiashara hao.
“Tutafurahi sana tukipata hiyo soko ya kuuza mboga na tutashukuru serikali kwa kusema inajali maslahi ya mwananchi wa kawaida,” aliongeza Onsano