Wakazi wa mtaa wa Mwembe wamepongeza serikali ya kaunti na idara ya barabara kwa kuweka matuta katika eneo hilo.
Wakiongea jumatatu na Hivisasa katika mtaa wa mwembe wadi ya Kisii ya kati eneo bunge la Nyaribari chache kaunti ya Kisii, walisema kuwa kuweka kwa matuta hayo kutasaidia sana kupunguza visa vya ajali za barabarani. Waliongeza kuwa waendeshaji magari na pikipiki hawana budi ila kupunguza mwendo ambapo awali walikuwa wanahatarisha maisha ya watu kwa kwenda kasi sana.
“Napongeza serikali ya kaunti ya Kisii na idara ya barabara kwa kusikia kilio chetu na kuweka matuta katika barabara hiii kwa kuwa ni muda mrefu sana tangu barabara hii itengenezwe bila kuwepo na matuta haya” Grace osoro, mkazi alisema.
Julius Mwangi, mwanabiashara katika mtaa huo wa Mwembe alisema kuwa kuvuka barabara hio hapo awali ilikuwa hatari sana hasa katika shughuli zao za kila siku za biashara zinazohusisha kuvuka kutoka upande mmoja hadi mwingine.
Aidha,wameomba serikali ya kaunti ya Kisii na idara ya barabara kusikia kilio cha wenzao wa Ogembo na kuweka matuta kama hayo kwani hata wao hutumia barabara hiyo haswa wakati wa kuenda kilgoris kwa ajili ya biashara.