Serikali ya kaunti ya Mombasa imeshtumiwa kwa kufanya miradi ya kuboresha miundomsingi kwa njia za mapendeleo na kutakiwa kutekeleza miradi hiyo kwa kila mtaa mjini humo.
Akiongea siku ya Jumapili kwenye mtaa wa Mkomani mjini Mombasa, mwanasiasa Saro Mbodze, ambaye ana azimio la kuwania kiti cha uwakilishi wadi cha Ganjoni, alisema kuwa serikali ya kaunti imeacha kuzibua na kukarabati mabomba ya kupitisha maji taka kwenye mitaa flani, na kusema kila mkazi katika kaunti ana haki ya kupewa huduma bora.
Saro alitaja ukosefu wa njia za kupitisha siweji kuwa chanzo cha wakazi wengi kupata maradhi ya kuumwa tumbo kwenye mitaa inayozingira mji wa Mombasa kama vile Likoni Simanzi, Kongowea na mitaa mingine ambayo ina idadi kubwa ya wakazi.
Kiongozi huyo alikuwa anawahutubia wakazi wa mtaa huo ambao walikuwa wanatoa lalama za kuvuja kwa maji taka na uwepo wa mazingira mabaya ya kufanyia kazi.
"Serikali ya kaunti sharti iwape wananchi huduma mhimu, majutaja ambayo yanavuja mara kwa mara kati mtaa huu ni ishara tosha kuwa serika haiwajibiki kwa umma," aliongeza kiongozi huyo.
Alisema mvua ambayo inanyesha italeta magonjwa kwa wakazi, ambapo aliitaka serikali kuangalia suala hilo kwa haraka.
"Kama hawatasikia kilio cha umma, nitawaongoza wakazi hawa kwenye maandamano hadi ofisi za gavana," alitishia Saro.
Baadhi ya wakazi ambao walizungumza katika mkutano huo walimtaka gavana wa kaunti ya Mombasa kuweka waangalizi katika kila mtaa na kutoa ripoti kuhusiana na uwepo wa hali ya miundomsingi katika mitaa yote kwenye kaunti hiyo.