Share news tips with us here at Hivisasa

Wakazi kutoka kaunti ya Mombasa wameitaka serikali kuwa wazi na kuwaelezea kinaga ubaga mahali ambako watatorokea wakati mvua ya El Nino itaanza kunyesha na kuwambia maeneo ya juu wanayosema ni wapi.

Baadhi ya wakazi hao kutoka maeneo ya Bouxton, na Tononoka ambayo huathiriwa sana hasa nyakati za mvua nyingi, waliongea na mwandishi huyu siku ya Alhamisi, walishangazwa na jinsi serikali kuu kupitia Wizara ya Majanga na Dharura pamoja na Idara ya hali ya anga imekuwa ikisisitiza mara kwa mara kuwa watu wahamie sehemu za nyanda za juu ilhali hizo nyanda za juu wanazoambiwa hawazijui.

Marium Abdallah, mkazi wa Tononoka alisema kuwa si sawa serikali kuendelea kuwaambia wananchi kila mara kuwa mvua ikianza waenda maeneo ya juu huku wengi wa watu hawaelewi ni nini wanamaanisha kwa maeneo ya nyanda za juu.

“Sisi tunasikia kua mvua ikiwa nyingi tuhamie maneo ya juu, sasa hatujui maeneo ya juu ni kwenye miti au nyumba za ghorofa. Ingekua vizuri serikali itenge mahali ambapo patafaa waathiriwa kuliko kuambia watu maeneo ambayo hawajui. Sharti wakazi waelezewe jinsi watajikwamua kutoka kwenye majanga ambayo yatajitokeza kufuatia mvua hiyo,” alisema Abdallah.

Mzee Ayubu Chome, ambaye ni mmliki wa majumba katika mtaa wa Bouxton, alisema kuwa eneo hilo limekuwa likiathiriwa mara kwa mara na anahofia kuwa huenda wakazi wengi wakajipata pagumu iwapo mvua hiyo itanyesha kama vile ilivyotabiriwa.