Serikali imetakiwa kutoa pesa za hazina ya Uwezo kwa watu binafsi wala si kwa vikundi kama inavyofanyika kwa sasa.
Akizungumza na mwanahabari huyu siku ya Jumapili, Salma Swaleh ambaye ni mkazi wa Kisauni alisema kuwa kina mama wengi na vijana wanaogopa kujiunga kwenye vikundi kwa sababu za kutoaminiana miongoni mwao hasa wakati wa ulipaji wa pesa hizo.
“Watu wengine hutoroka na kushindwa kulipa fedha hizo pindi tu wanapozitumia vibaya na kukosa faida ya kurejesha pesa hizo,” alisema Salma.
Aidha, aliongeza kuwa pesa hizo ni kidogo mno ikilinganishwa na gharama ya juu ya kuanzisha biashara nchini na kusisitiza kuwa serikali inafaa kuongeza fedha hizo.
Vile vile, alisisitiza kuwa ili maendeleo ya haraka ya kibiashara kupatikana, ni lazima sheria hiyo ya kuunda vikundi ifutiliwe mbali na pesa hizo zipewe mtu binafsi.