Share news tips with us here at Hivisasa

Afisa mmoja kutoka katika kitengo cha kuchunguza uhalifu alizua kizaazaa siku ya Jumanne katika mahakama kuu ya Mombasa kwa kususia kujibu maswali na kuwatuhumu wakili wa upande wa utetezi pamoja na mwendesha kesi moja ya dawa za kulevya kwa kudai kuwa walikuwa wanajirudia kwa kumuuliza maswali sawa.

Shahidi huyo kutoka kitengo cha kuchunguza uhalifu, ambaye ni wa pili kutoa ushahidi wake kwenye kesi hiyo, alionekana mwenye hasira pale wakili wa upande wa utetezi aliweza kutaja jina lake vibaya, na kumtaka aache kutetemeka, matamshi ambayo hayakumfurahisha shahidi huyo.

Shahidi huyo ambaye alitoa ushahidi wake kwa zaidi ya saa mbili na nusu alionekana kulemewa na mengi ya masuali aliyotakiwa kujibu kutoka upande wa mwendesha mashtaka na kutoka upande wa utetezi akidai kuwa yalikuwa maswali sawa na kila swali walilomuuliza lilikuwa kwenye faili zao na kwenye nakala ya OB aliyowasilisha mahakamani.

“Si nishasema na hayo unaniuza yapo katika hizo faili ziko mkononi wako, sisi hatufanyi kazi kama vile mnafanya, polisi wanafanya kazi tofauti na nyinyi, usitake nifanye vile mnafanya,” shahidi huyo alikema.

Hata hivyo, hakimu mkuu wa mahakama hayo, ambaye alikuwa anasikiliza kesi hiyo ya mihadarati, Richard Ondenyo aliweza kuingia kati na kutuliza hali baina ya pande hizo tatu ambazo zilidhihirika kuwa na tofauti baina yao, ambapo shahidi huyo baadaye aliweza kufanikiwa kumaliza kutoa shuhuda zake.