Usimamizi wa huduma za feri jijini Mombasa umetiwa lawama kwa mara nyingine kwa kuonyesha utepetevu wanaposhughulikia masuala ya misongamano kwenye kivuko cha Likoni baada ya watu kusongamana na kuvunja vizuizi na milango ya maeneo ya kungojea feri siku ya Ijumaa jioni.
Hali hiyo ambayo ilishuhudiwa kwa zaidi ya saa moja na nusu kuanzia saa kumi na moja jioni ilisababisha baadhi ya watu kukanyagana na wengine kujeruhiwa, japo kidogo, kwa kile kinachodaiwa kuwa uchache wa feri ambazo zinawahudumia watu pamoja na magari kwenye kivuko hicho.
Kulingana na Tom Helman ambaye ni mtalii kutoka Australia, alisitajabishia hali hiyo ambapo anadai waliweza kukaa kwenye mlolongo wa magari ambayo yalikuwa yanavuka kuelekea eneo ya South Coast, na kuwalaumu wasimamizi wa shirika kwa kukosa kuwajibikia wateja wao pamoja na wakazi.
Salma Mwinyi, mkazi eneo la Ganjoni alitoa wito kwa mamlaka ya feri KFS kutafuta ata kama ni feri moja mahususi ambayo itakuwa inashughulikia dharura kama ilishuhudiwa Ijumaa.
Aidha, alisema kuwa shirika linahitaji kuleta feri hata tatu mpya badala ya kutegemea feri ambazo tayari zimeonyesha dalili ya kuzeeka.
Shida hiyo ilishuhudiwa baada ya feri mbili ambazo zilikuwa zinahudumu kulemewa na kiwango pamoja na idadi kubwa na magari pamoja na watu ambao walikuwa wanavuka kutoka pande zote kutoka na kuingia kisiwani
Kulingana na mmoja wa wahudumu ambaye aliongea na mwandishi huyo, feri nyingine ambazo hudumu kivukoni zilikuwa na hitilafu ikabidi kuhudumu feri mbili.