Mfanyikazi wa Shirika la Msalaba Mwekundu amesema kuwa hakuna wakati ambao shirika hilo limeshurutishwa na serikali kuficha idadi ya watu ambao wamefariki katika ajali ama janga lolote lile.
Akizungumza na wanahabari siku ya Alhamisi, kwenye hoteli ya Legacy iliyoko Nakuru, Katika shughuli ya kutoa mafunzo kuhusiana na jinsi shirika hilo linavyofanya kazi, Jonuba Bekah, alisisitiza kwamba serikali haijawahi shinikiza shirika hilo kutotoa idadi ya watu ambao wameaga dunia katika janga.
Akiunga mkono usemi huo, Dkt Emmanuel Owako ambaye ni meneja wa Kaunti ya Nakuru wa shirika hilo, alisema kuwa kwa wakati mwingine, idadi ya watu ambao wameaga ambayo hutolewa na serikali na shirika hilo hutofautiana lakini akasisitiza kuwa idadi hiyo huwa haina tofauti kubwa.
Wakati huo huo, Bekah alisema kuwa Shirika la Msalaba Mwekundi na lile la St John Ambulance ni mashirika tofauti lakini hata hivyo, kwa wakati mwingine huwa mashirika hayo yanafanya kazi wa pamoja.