Shirika moja lisilo la kiserikali kutoka nchi ya Uingereza, 'Walking Against Poverty' (WAP) limeanza mradi wa kutoa matibabu ya bure kwa wakazi wa kaunti ya Nyamira.
Shirika hilo lilianza kutoa matibabu hayo jana siku ya Jumatatu, huku wakitembea katika sehemu mbalimbali kutoa matibabu hayo kwa wasiojiweza.
Baadhi ya magonjwa wanaopima na kutibu ni saratani, malaria na maumivu ya mgongo.
Mradi huo wa kutoa matibabu ya bure ni njia mojawapo ya kuwasaidia wale watu ambao hawajiwezi kufuatia umaskini.
Akizungumza na waandishi wa habari siku ya Jumatatu katika eneo la Borabu wakati walikuwa wanatoa matibabu hayo ya bure kwa wakazi, afisa mkuu anayesimamia shirika hilo Lawrence Ogot alisema watajaribu wawezalo kuhakikisha wametoa matibabu kwa wale wote ambao hawajiwezi ili kuzuia watu kupoteza maisha bure.
“Tuliamua tutoe matibabu kwa maeneo mbalimbali ya kaunti hii, maana tuligundua kuwa kuna watu wengi ambao hawawezi kugharamia matibabu yao. Tutawasaidia watu kama hao na hatuwalipishi chochote,”alisema Ogot.
Aidha, afisa wa mradi huo wa matibabu nchini Evans Obare aliomba watu kujitokeza kwa wingi ili kupimwa na kupokezwa matibabu ya bure katika sehemu zile watakazozuru.
“Tunaomba watu wajitokeze kwa wingi ili watibiwe maana matibabu haya yanatolewa ni ya bure,” alisema Obare.