Share news tips with us here at Hivisasa

Serikali ya kaunti ya Mombasa imesema kwamba shule zote katika kaunti hiyo zitaendelea na masomo kama ilivyoratibiwa hata baada ya serikali kutangaza kufungwa kwa shule zote nchini.

Kulingana na Waziri wa Elimu katika kaunti hiyo Tendai Lewa Mtana, hatua ambayo serikali imechukua inahujumu haki za wanafunzi pamoja na masomo yao, na akasema kuwa hatua hiyo huenda ikachangia pakubwa matokeo duni katika mitihani ya kitaifa.

Akiongea mjini Mombasa siku ya Jumamosi, Tendai alisema kwamba shule za umma, zile za kibinafsi, taasisi za kiufundi na chekechea zitaendelea na masomo kama kawaida, huku akisema kwamba serikali ya kaunti ya Mombasa itagharimu shughuli zote za masomo.

“Shule zote za umma na kibinafsi zitaendelea kama kawaida kwa sababu hatua ambayo serikali imechukua inahujumu haki za watoto kupata mafunzo ili kukamilisha malengo na ndoto za watoto katika siku za usoni,” alisema Tendai.

Amesema kwamba Serikali ya kaunti ya Mombasa imeandaa mikakati mwafaka ya kuwajumuisha wanafunzi wa shule zote za umma na kibinafsi katika juhudi za kuimarisha viwango vya elimu ili kuona kwamba watoto wanaorodhesha matokeo bora.

Tendai amehoji kuwa wadau wa sekta za shule za kibinafsi katika kaunti hiyo wamedai kutotii agizo la serikali kupitia baraza kuu la mitihani na wizara ya elimu kuagiza shule zote nchini kufunga, na akasema kuwa wamekubaliana na viongozi wa kaunti masomo kuendelea.

“Tulifanya kikao cha dharura na wadau wa sekta ya elimu katika shule zote za umma na kibinafsi katika kaunti ya Mombasa na tumekubaliana kaunti ya Mombasa masomo yataendela kama kawaida,” aliongeza Tendai.

Hatua hiyo imejiri baada ya serikali kutaka kufungwa kwa shule zote za umma na zile za kibinafsi kote nchini, baada ya walimu kudinda kurejea shuleni wakidai nyongeza yao ya asilimia 50 na 60.