Baada ya juhudi za Shule ya Msingi ya Kisii kitengo cha watoto wasio na uwezo wa kuongea na kuelewa al maarufu Autism kutaka kujisimamia, sasa imethibitishwa kuwa shule hiyo itasajiliwa hivi karibuni.
Thibitisho hilo limehakikishwa na mkurugenzi mkuu wa wanaoishi na ulemavu Isaac Rogito siku ya Ijumaa ambapo alisema tayari amewasilisha maombi ya kuandikishwa kwa shule hiyo (Autism Unit) ili kupata nambari ya kujisimamia kwa mamlaka husika ya usajili wa shule akiongeza kuwa utaratibu huo bado unaendelea.
Rogito aliongeza kuwa ushirikiano uliopo baina ya ofisi yake na mkuu wa shule hiyo ya msingi ya Kisii ni nzuri, hali ambayo alisema imechangia kuharakisha harakati ya usajili wa kitengo hicho hivi karibuni japokuwa hakubaini muda halisi shughuli hiyo itakamilika huku akisema shughuli hiyo ina utaratibu wa serikali na ni rasmi.
Mkurugenzi huyo ambaye pia anaishi na ulemavu wa macho alisema atafanya kila awezalo kuwakimu watu wote wanaoishi na ulemavu katika Kaunti ya Kisii na kuwataka kutembelea ofisi hiyo iwapo wana maswali au suala lolote kuhusiana na masuala ya ulemavu.
Vile vile, afisaa huyo aliwataka wazazi wote pamoja na wakazi wa Kisii wanao na watoto wanaoishi na ulemavu na watu walio na ulemavu kuhudhuria shughuli ya kujiandikisha na ofisi yake ambayo inaendelezwa na serikali kuu kuputia kwenye afisi za wilaya.