Idara ya watu wanaoishi na ulemavu katika Kaunti ya Kisii imeanzisha shule ya watu walio na ulemavu wa kuona katika eneo la Nyaribari Masaba, katika shule ya St Joseph Kiomiti.
Madarasa matatu yameanza kujengwa ili kuwafaa watu ambao hawana uwezo wa kuona na inatarajiwa kukamilishwa kabla ya mwisho wa mwaka huu.
Akiongea siku ya Jumatatu katika ofisi yake, mkurugenzi mkuu katika idara ya watu wanaoishi na ulemavu katika kaunti ya Kisii Bwana Isaac Rogito alisema kuwa tayari idara yake kwa ushirikiano na serikali kuu imetoa shilingi milioni mbili ili kuanzisha ujenzi huo.
Alisema kuwa hiyo ni shule ya kwanza katika kaunti ya Kisii ambayo itakuwa inawashughulikia watu walio na ulemavu wa macho, ambapo aliwataka wahusika kuchukua nafasi hiyo na kuanza kujiandikisha kwenye shule hiyo ambayo tayari masomo yanaendelea katika baadhi ya madarasa ambayo walikuwa wamepewa na shule hiyo ya Kiomiti.
"Wale wote ambao wana ulemavu wa macho sharti waanze kujiandikisha ili wajiunge na shule hiyo, kwa vile hii ni shule ya kwanza katika kaunti hii yetu ya Kisii," alisema Rogito.
Bwana Rogito ambaye pia ana ulemavu wa macho, alisema kuwa yuko katika harakati za kuhakikisha kuwa watu wote wanaoishi na ulemavu wa aina zote wanafaidi kutokana na miradi ambayo idara yake imeanzisha.
Aliwataka watu wanaoishi na ulemavu kumuunga mkono katika juhudi zake ili wapiganie haki zao kwa pamoja.
Alisema kuwa bado wanaendelea kushirikiana na serikali ya kaunti ya Kisii ili kuwanufaisha wahusika na kuitaka serikali kuu kuendelea kuwapa msaada wa kifedha ili kuhakikisha changamoto ambazo walemavu wanapitia zimepunguzwa.