Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Hata baada ya mahakama kuamuru walimu warejee darasani, shule nyingi za umma zimesalia mahame huku nyingine chache zikisajili idadi ndogo ya wanafunzu bila walimu kuwepo.

Kwenye pitapita katika shule za umma kwenye kata ya Nyamaiya, siku ya Jumatatu, tulipata kuwa shule ya msingi ya Nyamaiya ilikuwa na wanafunzi wachache watahiniwa wa darasa la nane huku shule ya msingi ya Ratandi na ile ya upili ya mseto ya Gekemoni zikisalia mahame.

Kulingana na mwanafunzi mmoja mtahiniwa wa darasa la nane kwenye shule ya msingi ya Nyamaiya, Peris Kemunto, baadhi ya watahiniwa wa mtihani wa kitaifa wa darasa la nane walifika shuleni mapema wakitarajia kupata huduma za walimu, lakini wakapata afisi zikiwa zimefungwa.

"Baadhi yetu, tulio watahiniwa wa mtihani wa kitaifa wa mwaka huu tulifika mapema humu shuleni lakini tukapata kufuli zikitukaribisha kwenye lango kuu la afisi,” alisema Kemunto.

Aidha, kulingana na naibu wa mwalimu mkuu wa shule moja ya upili ambaye jina lake limebanwa, walimu hawako tayari kurejea shuleni hadi pale matakwa yao yatakapo afikiwa.

"Walimu wa taifa hili hawako tayari kurejelea shughuli zao za kawaida hadi pale serikali itakapo afikia matakwa yetu,” alisema mwalimu huyo.

Lewis Nyakweba, katibu mkuu wa chama cha Kuppet tawi la Nyamira alisema kuwa ingawa jaji Nelson Abuodha aliamuru walimu kurejea madarasani, walimu wanachama wa muungano huo hawana hiari yakurudi shuleni kwa kuwa serikali haijatii agizo la mahakama ya rufaa yakuwapa nyongeza ya mishahara.

"Walimu wanachama wa muungano wa Kuppet tawi la Nyamira kamwe hawapo tayari kurejea madarasani hadi pale tume ya uajiri wa walimu itakapo tii agizo la nyongeza ya mishahara ya walimu,” alisema Nyakweba.

Katibu huyo alisema kuwa serikali ya kitaifa imekuwa ikiwadhalilisha walimu kwa muda sasa swala ambalo limewalazimu kugoma hadi pale matakwa yao yatakapo afikiwa.