Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Chama cha 'Kenya National Union of Teachers' (KNUT) tawi la Nyamira kimepongeza katibu mkuu wa chama hicho nchini Wilson Sossion kwa juhudi za kutetea walimu kupata haki yao.

Hii ni baada ya mahakama kuu kutoa uamuzi kuwa sharti walimu waongezewe mshahara wao kwa asilimia 50 hadi 60.

Akizungumza siku ya Jumatano mjini Nyamira, mwenyekiti wa chama cha KNUT tawi la Nyamira aliyeongea kwa niaba ya walimu wote wa kaunti hiyo Peter Mong’are, alisema Sossion amefanya jambo ambalo halitasahauliwa nchini kwa kutetea haki za walimu.

Aidha, mwenyekiti huyo aliomba tume ya kuajiri walimu nchini 'Teachers Service Commissioner (TSC) kuheshimu agizo la mahakama na kukubali kutoa pesa hizo kwa walimu mara moja la sivyo hawatarejea darasani mwezi ujao.

“Sisi walimu wa kaunti ya Nyamira tunampongeza katibu wetu kwa motisha aliokuwa nao tangu tuanze safari ya kupewa haki yetu na tunamwomba aendelee hivyo,” alisema Mong’are.

Matamshi ya mwenyekiti huyo ya kupongeza katibu wao yaliungwa mkono na viongozi wa chama cha KNUT wilayani Borabu kama Kiongozi wa Wanawake Eucabeth Bundi, Mwekahazina Charles Mogaka na Edward Omboingi huku wakiomba wazazi kuungana nao kupata haki yao ifikapo tarehe 31 mwezi huu.

“Hatutaenda darasani ikiwa TSC haitatupa pesa zetu na kuheshimu agizo la mahakama,” alisema Charles Mogaka, mwekahazina wa chama cha KNUT wilayani Borabu.