Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Spika wa bunge la kaunti ya Nyamira Joash Nyamoko amesema kuwa atasubiri kesi ya mwakilishi mteule katika bunge hilo Doris Nyabiage kukamilika ili kutangaza nafasi ya mwakilishi huyo kuwa wazi au la.

Hii ni baada ya mwakilishi huyo wa chama cha Kenya Social Congress kushtakiwa kwa madai ya kutumia vyeti vya masomo vya mtu tofauti ambavyo si halali wakati aliteuliwa kuwa mwakilishi wadi mteule katika kaunti ya Nyamira

Norah Bisibori Amenya anadai kuwa mwakilishi huyo alitumia vyeti vyake vya masomo, jambo ambalo alimshtaki nalo katika mahakama ya Nyamira.

Akizungumza siku ya Jumanne katika vikao vya bunge la kaunti ya Nyamira, Nyamoko alisema hawezi kutangaza nafasi hiyo kuwa wazi kabla ya kesi inayomkabili mahakamani kukamilika.

“Kesi ikikamilika nitakuwa na nafasi nzuri ya kutangaza nafasi ya mwakilishi huyo kuwa wazi au la, lakini kwa sasa wacha tusubiri uamuzi wa mahakama kwanza,” alisema Nyamoko.

Mwakilishi huyo mteule anasisitiza kuwa vyeti hivyo vya masomo alivyotumia ni vyake, na kusema yuko tayari kutumikia wananchi wa kaunti ya Nyamira kimaendeleo

Kesi ya mwakilishi huyo na yule anadai kuwa alitumia vyeti vyake ilisikizwa jana, Jumanne, katika mahakama ya Nyamira.

Wakati huo huo, mwakilishi huyo, kupitia wakili wake Steve Mogaka aliomba mda zaidi kujitetea kabla ya kesi hiyo kukamilika, jambo ambalo jaji wa mahakama hiyo ya Nyamira Chrispene Agila alikubali na kuwaongeza mda.

Tarehe ya kusikizwa kwa kesi hiyo itatangawa baadaye baada ya mahakama ya vyama vya kisiasa nchini na mahakama ya Nyamira kujadiliana na kutafuta tarehe halisi.