Spika wa bunge la Kaunti ya Nyamira Joash Nyamoko amepuuzilia mbali madai ya mbunge wa Mugirango Kaskazini Charles Geni, kuwa anahujumu miradi ya maendeleo.
Akiongea siku ya Jumamosi alipokuwa akifanya mkutano na vijana wa eneo bunge hilo nyumbani kwake kule Nyamusi, Nyamoko alisema kuwa mbunge wa eneo hilo anamlaumu bure kuhusiana na kuingililia kwake miradi ya maendeleo.
"Sikatai kwamba mimi ni mkazi wa eneo bunge la Mugirango Kaskazini na nina nia yakugombea kiti cha eneo bunge hilo, lakini madai ya mbunge wa sasa kuwa nahujumu miradi yake ya maendeleo ni ya uongo na hayana msingi wowote," alisema Nyamoko.
Nyamoko aliongeza kuwa yafaa mbunge wa sasa Charles Geni awe tayari kupambana na pingamizi za wananchi wa eneo hilo ambao hawajaridhishwa na uongozi wake badala yakutafuta vizingizio.
"Yafaa Mbunge Geni awe tayari kupambana na pingamizi za wananchi kuhusiana na kutoridhishwa na uongozi wake badala yakutafuta vizingizio ili kukwepa hali halisi ya mambo," alisema Nyamoko.
Nyamoko alisema kuwa yafaa Geni awahusishe wananchi katika maamuzi mbalimbali ya maendeleo ili wapate fursa yakuchangia kwenye miradi mbalimbali.
"Kiongozi mzuri ni yule aliye tayari kuwapa nafasi wananchi kuchangia kwenye maamuzi ya kufanya miradi mbalimbali. Kwa mfano, yafaa mheshimiwa Geni awe tayari kuwapa sikio wananchi ili kujua mbona baadhi yao wanataka mradi wa maji wa Matongo uhamishiwe Nyaramba," alisema Nyamoko.
Spika huyo vilevile aliwasihi wabunge wa kaunti ya Nyamira kushirikiana pamoja na wawakilishi wa wadi katika kuleta maendeleo mashinani.
"Ningependa kuwasihi wabunge wa kaunti ya Nyamira kuwa tayari kuwashirikisha wawakilishi wa wadi kwenye miradi mbalimbali ya maendeleo, kwa kuwa viongozi wote tuliopo sasa tuliteuliwa ili kusaidia wananchi kujiendeleza," alisema Nyamoko.
Mbunge wa Mugirango Kaskazini Charles Geni alikuwa amemshtumu Spika Nyamoko kwa kuwachochea wananchi kupinga miradi mbalimbali ya maendeleo.