Spika wa bunge la Kaunti ya Uasin Gishu Isaac Terer amesema kuwa Wakenya wanatakiwa kuwasheherekea maafisa wa usalama kama mashujaa.
Akizungumza siku ya Jumanne katika uwanja wa 64 huko Eldoret katika sherehe ya kuadhimisha siku ya Mashujaa, Terer alisema kuwa vyombo vya usalama vinasaidia katika uimarishaji wa usalama nchini na kuleta amani.
“Maafisa wetu wa polisi wanafanya kazi usiku na mchana ili kuhakikisha usalama wa kila mwananchi uko sawa. Leo hii tunawasheherekea," alisema Terer.
Aliwapongeza haswa wale ambao wako nchini Somalia kukabiliana na magaida wa al-Shabaab.
"Nawapongeza wazazi wa vijana hao kwa kukubali wanao wapiganie nchi yetu," alisema Terer.
Naibu Gavana wa Kaunti ya Uasin Gishu Daniel Chemno kwa hotuba yake aliwataja wanariadha wa kaunti hiyo kama mashujaa, kwa kuwa wamechangia pakubwa katika kuiwakilisha nchi ya Kenya.
"Tunawasherehekea wale wote ambao wamechangia katika kukuza uchumi wa nchi hii," alisema Chemno.