Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Baraza kuu la Waislamu nchini Supkem limesema kwamba Wakenya Waislamu walioenda kuhiji nchini Saudia Arabia wako salama.

Hii ni baada ya tetesi kuzuka kuwa baadhi yao walikuwa kati ya Waislam walioaga dunia katika mkanyagano uliyoshuhudiwa siku ya Alhamisi.

Kulingana na Mwenyekiti wa Baraza hilo nchini, Profesa Abdulghafur El-Busaidy, Waislamu kote duniani walihuzunika kufutaia maafa hayo yaliyoshuhudiwa mahujaji walipokuwa wakishiriki moja ya nguzo muhimu za mwisho katika ibada ya hija.

Akizungumza mjini Mombasa siku ya Alhamisi, El-Busaidy alisema kwamba Wakenya Waislamu waliosafiri nchini humo wako salama na akawahimiza Waislam humu nchini kuwaombea wenzao waliyokwenda kuhiji ili Mwenyezi Mungu awajalie warudi salama.

“Wakenya waliyosafiri Mekka nchini Saudia Arabia kuhiji wako salama. Tungepanda kuwahimiza Waislamu kote nchini kuzidi kuwaombea wenzetu warudi salama na tafadhili muondoe hofu kwani ndugu zetu wako salama,” alisema El-Busaidy.

Kwa upande wake, Kadhi Mkuu Sheikh Sharrif Muhdhar, aliwahimiza Wakenya kuwa na ushirikiano mwema na kuzidi kuwaombea wenzao waliokwenda kuhiji kuwa salama huku akiwataka kuwa katika mstari wa mbele kuenza amani.

“Ningependa kuwahimiza Waislamu tuzidi kushirikiana kwa karibu mno pamoja na ndugu zetu Wakristu kwani sote ni wamoja na tuwaombee ndugu zetu walioenda Mekka kuhiji,” alisema Sheikh Muhdhar.

Mkasa huo ni mkubwa zaidi kutokea katika kipindi cha miaka 25 huku Rais Uhuru Kenyatta akituma risala za rambirambi kwa serikali ya Saudi Arabia na jamii ya kiislam kwa jumla kufuatia maafa hayo.