Naibu Mwenyekiti wa Chama cha Maendeleo ya Wanawake Kaunti ya Mombasa amesema swala la misimamo mikali miongoni wa vijana wadogo wanaojihusisha katika ugaidi na uhalifu litatuliwe kwa haraka ili kuwanasua vijana hao.
Akizungumza mjini Mombasa siku ya Jumatatu, katika kongamano la wanawake la kujadili mbinu tofauti za kusitisha maswala ya misimamo mikali na kuimarisha usalama Bi Sureya Hersi alisema kwamba swala la misimamo mikali miongoni wa vijana linafaa kutafutiwa suluhu la kudumu kwa kuwahamasisha vijana kuhusu umuhimu wa uiano na utangamano iwapo serikali, viongozi wa kidini na jamii katika taifa hili wanahitaji usalama.
“vijana wetu wadogo wamehadaiwa na kujiunga na ugaidi kutokana na kushawishiwa mambo ya uovu na kuwa na msimamo mkali. Hali hiyo imekuwa tishio kubwa kwa usalama wetu na lazima suluhu la kudumu lipatikane,” alisema Sureya.
Aidha, amewahimiza vijana kujitenga na baadhi ya watu wanao walaghai kwa kuwapa fedha ili kujiunga na ugaidi na kurithi swala la misimamo mikali ili kuvuruga usalama wa taifa hili.
“Tunawaomba vijana wetu wasikubali kudanganywa na watu fulani na kuharibu ndoto zao kwa kujiungana na ugaidi kwa madai kuwa hakuna kazi. Kazi ziko na serikali iko tayari kuwapa kazi.Tafadhali akina mama tuwashauri watoto wetu,” aliongeza Bi Sureya.
Kauli ya Kiongozi huyo inajiri huku kaunti ya Mombasa ikikumbwa na msukosuko wa ukosefu wa usalama baada ya mshukiwa mmoja wa ugaidi kukwepo mtego wa maafisa wa polisi na kuwaacha wakazi wakiwa na hofu ya usalama.