Hata baada ya Idara ya utabiri wa hali ya anga nchini kuwahimizwa wakazi wanaoishi katika maeneo ya mabonde kuhamia nyanda za juu na kuepukana na mvua ya El Nino, tahadhari hiyo haijazingatiwa.
Hii ni baada ya kushuhudiwa kunyesha kwa mvua kubwa na kusababisha maporomoko ya ardhi na mafuriko katika maeneo ya wakazi hapo awali.
Kulingana na Mkurugenzi wa Idara hiyo katika Kaunti ya Mombasa, Lydia Kinoti, huenda mvua hiyo ya El Nino ikafikia viwango vya mililita 250 katika kaunti hiyo, hali itakayo kuwa hatari na huenda ikaathiri maeneo mengi ya kaunti hiyo.
“Tunatarajia mvua kubwa zaidi msimu huu wa viwango vya mililita 250 ambayo ni hatari sana kwa wakazi wanaoishi katika maeneo ya mabonde. Hata hivyo, tunashangazwa na jinsi wakazi wanavyochukulia tahadhari hii,” alisema Lydia.
Akizungumza mjini Mombasa siku ya Jumanne, Kinoti alisema kwamba kwa ushirikiano na wadau wengine katika kaunti hiyo, wametenga vituo vya kuwasaidia waathiriwa wa mvua ya El Nino katika Shule ya Upili ya Kajembe, eneo la Changamwe, Kituo cha kuzima moto katika eneo la Likoni, Uwanja wa Tononoko eneo la Mombasa na Uwanja wa maonyesho ya kilimo eneo la Kisauni.
Kinoti aliwatahadharisha wakazi wanaoishi katika vitongoji duni vya Moroto eneo la Tudor, Kalahari eneo la Changamwe, Junda na Mishomoroni eneo la Kisauni na Shell Beach eneo la Likoni na maeneo mengine kuyahama maeneo hayo ili kuepukana na majanga.
“Ni lazima wakazi wahame maeneo hayo kwani huenda mvua hiyo ikaleta hata maafa na majanga makubwa iwapo wakazi watazidi kupuuzilia mbali tahadhari hiyo. Tafadhali wasingoje mpaka mafuriko yatokee ndio waanze kuhama. Tungependa kuona wakianza wakati huu ili kuepukana na majanga,” alisema Kinoti.
Mvua hiyo ya El Nino imetabiriwa kuanza kunyesha mwezi huu wa Oktoba hadi mwezi wa Januari mwaka ujao.