Spika wa bunge la Kaunti ya Uasin-Gishu Bw Isaac Terer ametaka maafisa wa serikali ambao wanatuhumiwa kuhusika katika ufisadi kujiuzulu.
Akizungumza siku ya Jumanne wakati wa maadhimisho ya siku ya mashujaa mjini Elodret, katika uwanja wa 64, Bw Terer alisema ufisadi ambao umekita mizizi nchini umekosea heshima mashujaa ambao waliletea Kenya sifa.
Terer amezitaka taasisi za kukabiliana na ufisadi nchini kunoa makali yake na kukabiliana na ufisadi vilviyo.
Spika Terer alitaka taasisi hizo kupewa nafasi ya kufanya kazi husika bila kuingiliwa kisiasa.
Akirejelea sakata ya hivi maajuzi katika shirika la huduma ya vijana kwa taifa NYS, Bw Terer alitaka watuhumiwa katika ufisadi huo kujiuzulu pamoja na maafisa wote wakuu katika wizara husika.
“Watuhumiwa wote wa ufisadi ni sharti wajiuzulu bila kulindwa na mtu yeyote yule, pasipokujali tabaka la mhusika serikalini,” alisema Bw Terer.
Spika huyo aliuliza ni vipi utawala wa kaunti utakabiliana na ufisadi, ilihali ufisadi huo upo katika afisi ya rais.
Bw Terer alisema kukita mizizi kwa ufisadi nchini kunachangia katika changamoto ya kuduwaa kwa uchumi.
Kiongozi huyo alisema ufisadi unazidi kurudisha maendeleo nyuma kote nchini.
“Ili kuafikia ufanisi katika vita dhidi ya ufisadi, Wakenya wa matabaka yote wanapswa kuwa makini na kufuatilia namna viongozi wanavyotumia raslimali ya umma,” alisema Terer.
Aliongeza, “Nyinyi wananchi mna haki ya kufuatilia kwa makini namna viongozi wanavyotumia mali ya umma kwani ni haki yenyu kikatiba.”