Chama cha TNA Tawi la Nakuru kiliandaa hafla ya maombi siku ya Jumamosi katika Bustani ya Nyayo Gardens mjini Nakuru, ili kuombea Naibu wa Rais William Ruto na mtangzaji Joshua Arap Sang.
Viongozi wa madhehebu mbali mbali ya kikristu pamoja na wahubiri wa Kiislamu waliongoza mamia ya waumini katika maombi hayo, yaliyohudhuriwa na wakenya wa tabaka mbali mbali.
Akizungumza kabla ya maombi hayo, kiongozi wa chama cha TNA Nakuru Dkt Abdul Noor, alisema kwamba ukabila katika Kenya ni lazima uangamizwe, ili taifa hili lisishuhudie umwagaji wa damu.
“Tumekusanyika hapa kuombea naibu wetu wa rais, pamoja na mtangazaji Joshua arap Sang, kwa sababu ni wakenya kama sisi, na kila mtu anaweza kujipata na shida. Kama tunataka kusonga mbele, tafadhali tuwachane na maswala ya ukabila,” alisema Noor.
Viongozi hao wa kidini hata hivyo walikemea wanasiasa kwa kile walichokitaja kama kujipenda kupita kiasi, na kuwaomba kuzingatia maswala ya mwananchi wa kawaida.
Viongozi wa kiisalmu waliokuwemo ni pamoja na Issa Gichangi na Sheikh Adhman Masud kati ya wengine.
Maombi hayo yanajiri katika msururu wa maombi yanayaonadaliwa nchini na viongozi wa Jubilee katika maeneo tofauti ya Kenya, kudhihirisha umoja wao katika kukemea kesi dhidi ya Ruto katika mahakama ya jinai ICC.