Wanachama wa TNA kaunti ya Nakuru wamewalai walimu kusitisha mgomo na kurejelea majukumu yao.
Pia wameitaka serikali kuwapa walimu nyongeza ya mishahara kwa awamu ili kukwepa kuadhiri uchumi wa nchi pamoja na mapato ya serikali.
Kupitia mwenyekiti wa chama hicho Harrison Muiruri, wanachama hao wamesema wakati umefika kwa vyama vya kutetea haki za walimu pamoja na idara husika za serikali kushauriana na kuafikiana ili wanafunzi waendelee na masomo yao pamoja na matayarisho ya mtihani wa kitaifa wa KCSE na KCPE.
“Wanafunzi wa shule za umma wanaendelea kuteseka wakiwa nyumbani badala ya kuwa shuleni. Tunafahamu hatua zinazochukuliwa na serikali na kwa hivyo tungependa walimu pamoja na vyama vyao kuwa wazalendo na kufanya mashauriano ya kudumu na serikali,’’ alisema Muiruri.
Wakiongea kutoka Elburgon baada ya kufanya mkutano wa wanachama, viongozi hao wamesema swala la nyongeza ya mishahara ya walimu liliibuka tangu miaka ya tisini na walimu wamekuwa wakipata nyongeza ya mishahara tangu wakati wa serikali ya rais wastaafu Daniel Moi na Mwai Kibaki.
Aidha, wanachama hao wametoa wito kwa wakenya kujiepusha na kuchangia walimu pesa kwa minajili ya nyongeza wanayopigania. Wamesema walimu, kama wafanyikazi wa serikali, hawafai kupewa msaada kama inayopendekezwa na viongozi wa mrengo wa Cord.
Tetesi kama hizo zimetolewa na viongozi wa vijana katika eneo la Elburgon wakiongozwa na Moses Muiru ambaye amesema viongozi wa Cord hawajatoa maelezo ya jinsi pesa wanazochangisha zitakavyo wafikia walimu.
“Wanasiasa wa Cord wanafaa kuwaeleza wakenya jinsi pesa wanazokusanya zitakavyo wafikia walimu kwa sababu huenda hii ni njama ya kutafuta hela za kufanya kampeini ya 2017. Iwapo serikali itawalipa walimu hizi pesa zitapelekwa wapi? aliuliza Muiru.