Tume ya kuajiri walimu nchini TSC, imekosolewa kwa kutoheshimu agizo la mahakama la kuwalipa walimu mshahara wao wa mwezi wa Septemba.
Mahakama iliagiza TSC kutowachukulia walimu hatua yoyote kufuatia mgomo waliokuwa nao na kuwalipa walimu mshahara wa mwezi wa tisa.
Akizungumza na waandishi wa habari siku ya Jumapili mjini Kisii, msimamizi wa chuo kikuu cha Jaramogi Oginga Odinga University of Science and Technology (JOOUST) tawi la Kisii, ambaye pia ni mwanakamati katika bodi ya elimu katika kaunti ya Kisii, Dkt Henry Onderi, alikosoa tume ya TSC kwa kutowalipa walimu na kuagiza tume hiyo kufuata agizo la mahakama na kuwalipa walimu mshahara wa mwezi wa Septemba.
Onderi alisema huenda sekta ya elimu ikaathirika ikiwa walimu hawatalipwa mshahara wao kwani wengi wa walimu wamekufa moyo na kupoteza imani kwa mwajiri wao.
“Naomba tume ya TSC iwache kuwasumbua walimu na iwalipe mshahara wao wa mwezi wa Septemba. Walimu walionyesha heshima na wakarudi kazini mbona tume ya TSC isionyeshe heshima na iwalipe? alisema Onderi.
Aliongeza, “Tumesikia wengine wameanza kujitoa uhai kwa kutolipwa mshahara. Tutaongojea wote wajitoe uhai kweli? Tume hiyo inapaswa kujaribu iwezalo iwalipe walimu mishahara yao.”
Onderi pia alisema serikali ilitenga pesa nyingi kupambana na mvua ya El Nino huku akiomba pesa hizo zitumike kuwalipa walimu.