Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Katibu mkuu wa muungano wa walimu Knut tawi la Kilindini Dan Aloo ameitaka tume ya kuajiri walimu nchini TSC kuwalipa walimu mishahara yao ya mwezi Septemba kama ilivyoagizwa na mahakama la sivyo wasimamishe shughuli za masomo mara moja.

Aloo ameilaumu tume hiyo kwa kukaidi agizo la mahakama hatua aliyosema imeathiri shughuli nyingi zikiwemo walimu kushindwa kuwapeleka watoto wao shuleni pamoja na chama cha Knut kukosa fedha za kuendesha shuguli zake za kitaifa.

Aidha, katibu huyo alitaka serikali kutoa fedha za elimu ya bure katika shule za umma nchini akisema kucheleweshwa kutolewa kwa fedha hizo kunatishia kusambaratisha shughuli za shule hizo.

Vilevile Aloo alielezea imani ya walimu kushinda kesi yao ilioko mahakamani kwa sasa ya kutaka wapewe nyongeza ya mishahara yao ya kati ya asilimia 50-60 na kuwataka walimu kuendelea na shuguli za masomo wanaposubiri uamzi wa mwisho.

“Nina imani kuwa tutashinda kwenye kesi ambayo iko mahakamani na walimu tieni bidii kuwafundisha wanafunzi,” Aloo alisema.