Share news tips with us here at Hivisasa

Tume ardhi nchini NLC huenda ikavunjiliwa mbali iwapo bunge la kitaifa litapisha mswada uliowasilishwa bungeni kuvunja tume hiyo.

Kuvunjwa kwa kamati hiyo ni kwa madai ya kushindwa kutatua mizozo ya ardhi nchini.

Kulingana na mwenyekiti wa NLC Dkt Mohammad Swazuri, kuna baadhi ya viongozi walio na njama potovu na wanalenga kuvunjwa kwa tume hiyo kupitia Omnibus Amendment Bill.

Akiongea mjini Mombasa siku ya Jumamosi katika vikao vya kukusanya malalamishi ya mizozo ya ardhi kwa wakazi wa eneo bunge la Mvita kaunti ya Mombasa, Swazuri alisema kwamba tume hiyo iko huru kikatiba na wananchi pekee ndio wenye uwezo wa kuivunja kutumia kura ya maamuzi.

“Bunge haliwezi kuvunjilia mbali tume ya ardhi kwa sababu si kikatiba. Kuna wenye malengo yao binafsi wanaotaka kurudisha nyuma maendeleo ya nchi iwapo mswada huo utapitishwa,” alisema Swazuri.

Swazuri amesema kwamba kwa sasa, wizara ya ardhi inafanya kila juhudi kupunguzia mamlaka tume hiyo bila ya kuegemea kura ya maamuzi.

Mbunge wa Mvita Abduswamad Sharif Nassir amesema kwamba baadhi ya wizara nchini zinashinikiza kupunguziwa mamlaka tume hiyo ili ziendeleze ufisadi.

“Wapo baadhi ya maafisa katika wizara za serikali waliyo na njama ya kupunguziwa mamlaka tume ya ardhi. Viongozi wa Pwani tutasimama kidete kupigania tume hiyo isivunjwe,”alisema Nassir.