Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Tume ya ugavi wa rasilimali nchini CRA imewashtumu wawikilishi wa wadi kwa kushindwa kutekeleza majukumu yao ya kuhakikisha kwamba serikali za kaunti zinazingatia sheria katika utendakazi wao.

Akizungumza katika kikao cha kuwahamasisha wawakilishi wa wadi wa bunge la Kaunti ya Nyamira kwenye mkahawa mmoja mjini humo siku ya Jumatano, Naibu Mwenyekiti wa tume hiyo Fatuma Abdulkadir alisema kuwa wawakilishi wa wadi ndio wanaofaa kuwajibikia uvujaji wa pesa katika serikali za kaunti.

"Wawakilishi wadi ndio wanaofaa kuwajibikia vitendo vya uvujaji pesa katika serikali za kaunti kwa kuwa wao ndio hawatekelezi majukumu yao ipasavyo,” alisema Bi Abdulkadir.

Abdulkadir aidha alipinga vikali matakwa ya wawakilishi wadi yakutaka kupewa pesa za hazina ya maendeleo wadi huku akisema kazi ya wawakilishi wadi nikuchunguza kuhakikisha shughuli zinaendeshwa vizuri na wala sio kuzitekeleza.

Spika wa bunge la Kaunti ya Nyamira Joash Nyamoko alishangazwa na ukosefu wa serikali ya kaunti ya Nyamira kutotekeleza miradi mbalimbali kwa wakati unaofaa hata baada ya bunge kutenga pesa zakufadhili miradi hiyo.

"Ninashangazwa na ni kwa nini baadhi ya miradi muhimu hasa ile yakuanzishwa kwa chuo kikuu haijatekelezwa hadi sasa hata baada ya bunge kuidhinisha bajeti yakufadhili miradi hiyo,” alisema Nyamoko.

Kiongozi wa walio wengi kwenye bunge la kaunti ya Nyamira Laban Masira aliilaumu tume ya ugavi wa raslimali CRA kwa kuipa kaunti ya Nyamira mgao wa chini wa fedha hata kuliko kaunti zingine zilizo na idadi ndogo ya watu.

"Tume ya ugavi wa raslimali ilitengea Kaunti ya Nyamira kiasi kidogo cha pesa hata kuliko kaunti zingine zenye idadi ndogo ya watu, hali inayosababisha iwe vigumu kwa serikali yetu kutimiza malengo yake," alisema Masira.