Serikali ya kaunti ya Kisii imeweka mikakati kabambe ya kuhakisha kuwa wakulima wa kaunti hiyo watafaidika na miradi mbalimbali ili kujiendeleza na kilimo katika kaunti hiyo.
Akizungumza siku ya Ijumaaa katika uwanja wa Gusii katika hafla ya maonyesho ya kilimo ambayo yanaendelea anayesimamia sekta ya kilimo katika kaunti ya Kisii Vincet Sagwe aliwahakikishia wakulima kuwa serikali ya kaunti imeweka mikakati ambayo itawasaidia wakulima kujiendeleza na ukulima na ufugaji katika kaunti ya Kisii.
Sagwe alisema kuwa serikali ya kaunti ya Kisii ikiongozwa na Gavana James Ongwae imepea kilimo nafasi ya kwanza kwa kuwa kilimo ndio uti wa mgongo wa kaunti hiyo.
“Kilimo ndio uti wa mgongo katika kaunti yetu kwa hivyo tumeweka mikakati kabambe ya kuhakikisha kuwa kilimo kinaendelea bila tashwishi yoyote katika kaunti yetu,” alisema Sagwe.
Kati ya mikakati iliyowekwa ni kuhakikisha kuwa wafugaji wa ng’ombe wamepata mafunzo bora ya jinsi ya kufuga ng’ombe wa maziwa ili kupata faida ya kujiendeleza.
Kwa upande mwingine, aliwaomba wakulima wawe wanachukulia masuala ya kilimo kwa makini kwani kilimo ndio suluhu ya janga la njaa katika nchi.
“Nawaomba wakulima kuchukulia mafunzo haya wanayopata kutoka maonyesho haya ya kilimo kwa makini ili waweze kuyatumia wakati wanapofanya kilimo chao nyumbani,” aliongezea Sagwe.
Kwa upande wake, Gavana wa kaunti ya Kisii James Ongwea alisema kuwa serikali yake itahakikisha kuwa kilimo kimepewa kipaumbele ili kuinua uchumi wa kaunti ya Kisii.