Share news tips with us here at Hivisasa

Mkurugenzi mkuu wa shirika la kijamii maarufu kama ‘Kenya Community Support Centre’ Phyllis Muema amesema kwamba ugatuzi haujawapa vijana kipaumbele katika maswala ya ajira na kuchangia hali ngumu ya maisha.

Akiongea katika warsha wa kuadhimisha siku ya amani duniani mjini Mombasa siku ya Jumatatu, Muema amesema kwamba ukosefu wa usalama unaoshuhudiwa katika kaunti ya Mombasa na kwengineko Pwani umechangiwa na ukosefu wa ajiri miongoni mwa vijana.

Kulingana na Muema, ni jukumu la viongozi na wadau wengine kujitolea kikamilifu katika kuangazia vyema ugatuzi ili kumfaidi kijana mashinani, huku akihoji kwamba iwapo swala hilo litazingatiwa na kutoa nafasi za ajiri kwa vijana kutasaidia pakubwa kuzuia kukithiri kwa visa vya kihalifu.

“Sisi kama viongozi tunafaa kijitolea kikamilifu katika kuangazia ugatuzi mashinani ili kumfidia kijana na jamii kwa jumla katika maswala ya kimaendeleo kwa kubuni nafasi za ajira kwa vijana wetu. Hatua hiyo itasaidia pakubwa kupuuza kuenea kwa visa vya uhalifu,” alisema Muema.

Aidha, amesema kwamba kwa sasa shirika hilo limo nyanjani na kutoa hamasa kwa vijana na jamii kwa jumla jinsi ya kufahamu umuhimu wa ugatuzi na kujihusisha na vikundi vya kimaendeleo ili kupata usaidizi kutoka kwa mashirika na kujikimu kimaisha.

“Tayari tumeanza kutoa hamasa kwa vijana na jamii kwa jumla huko mashinani kama njia mojawapo ya kuwaelemisha vijana na jamii kufahamu mengi jinsi ya kufanya maendeleo na kujikimu kimaisha. Naona hatua hiyo tutakuwa tumewajibikia vyema ugatuzi,” aliongeza Muema.

Zaidi ya vijana 100 wanaendelea kupata mafunzo ya kijihusisha na miradi mbalimbali ya kimaendeleo katika eneo zima la Pwani ili kuona kwamba vijana hawajihusishi na masaula ya uhalifu na mihadarati.