Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Uongozi wa shamba la makonge lililo Rongai, umepatiwa siku 21 kuhakikisha kuwa maswala mbalimbali muhimu kama vile uwepo kwa vyoo vya kutosha kwa wafanyikazi yanazingatiwa au washtakiwe.

Notisi hiyo iliyotolewa kwa uongozi huo wa shamba la Alphega Mogotio Plantations na kutiwa saini na afisa wa afya ya umma kwenye kaunti ya Nakuru Samwel king’ori siku ya Alhamisi.

Notisi hiyo ilisema kuwa shamba hilo lina vyoo visivyo visafi, vilivyo na kasoro na ambavyo havitoshi kwa matumizi ya wafanyikazi wa shamba hilo.

Idara hiyo ya afya ya umma pia ilitaja ukosefu wa bomba la kuondoa maji machafu yanayotoka kwenye bafu na umwagaji wa maji machafu hadharani kama sababu ambazo huenda zikapelekea uongozi wa shamba hilo kushtakiwa.

Isitoshe, makaazi duni, vichaka vilivyomea pakubwa na ukosefu wa maji masafi pia yametajwa kama baadhi ya sababu ambazo huenda zikapelekea hatua hiyo kuchukuliwa.

Kutokana na hilo, King’ori ameagiza uongozi wa shamba hilo kujenga vyoo saba vipya katika muda huo wa siku 21, pamoja na kufyeka vichaka hivyo na pia kuhakikisha kuwa kuna maji safi na kuwa makazi yote ya wafanyikazi hao yanatengezwa.

Pamoja na hayo, uongozi wa shamba hilo umetakiwa kujenga bafu za kudumu ambazo zitakuwa na mabomba ya kutoa maji taka na pia kutoa huduma za ambulensi kwa wafanyikazi.

Matamshi haya yanajiri baada ya taarifa kuzuka kuwa ugonjwa wa kipindupindu ulizuka katika kaunti ndogo za Mogotio na Rongai, huku ikibainika kuwa watu wanne waliolazwa hospitalini kutokana na ugonjwa huo ni wafanyikazi wa shamba hilo.

Kulingana na Mkurugenzi wa Kaunti ya Nakuru katika sekta ya huduma ya afya Dkt Joseph Lenai, aliyezungumza hapo awali na wanahabari, hatua ya watu kujisaidia katika shamba hilo la makonge pia limepelekea vijidudu vya ugonjwa huo kusambaa hadi kwa mto Molo, jambo lililo sababisha mkurupuko wa ugonjwa huo.

Hivyo basi, ametaka umma kuchukua hatua za dharura na zinzotolewa na maafisa wa afya ili kuzuia kupata ugonjwa huo.