Mamia ya wanafunzi wamewasili katika Chuo Kikuu cha Moi Bewa kuu kusajiliwa kwa mwaka wao wa kwanza katika shughuli iliyoanza siku ya Jumatatu.
Chuo hicho ambacho husifika kwa kusajili idadi kubwa ya wanafunzi wanaojiunga na vyuo vikuu vya umma kimeshuhudia mamia ya wanafunzi kutoka sehemu mbalimbali nchini wakiwasili tayari kujiunga na chuo hicho.
Akizungumza na wanahabari siku ya Jumatatu, mkuu wa shule ya Ujenzi wa Raslimali, Ruth Tubey, alielezea furaha yake kwa kupokea wanafunzi wengi mwaka huu.
“Tunafurahia kuwa wanafunzi wamejitokeza kwa wingi hii leo na ninachukua fursa hii kuwakaribisha kwenye shule hii,” alisema Tubey.
Tubei alisema kuwa huu ndio mwaka ambao shule hiyo imesajili wanafunzi wengi zaidi.
“Mwaka huu tunafurahia kuwa wanafunzi wengi walichagua kujiunga na shule hii. Tunatarajia zaidi ya wanafunzi mia sita,” alisema Tubey.
Baadhi ya wanafunzi na wazazi pia wamefurahia namna shughuli hiyo inavyoendeshwa licha ya changamoto za foleni ndefu na jua kali.
Chuo hicho kilizindua mtindo mpya ambao wanafunzi hutafuta nyumba mtandaoni na kupunguza idadi ya foleni na visa vya utoaji rushwa katika kupata nyumba.
Shughuli hiyo ilianza rasmi siku ya Jumatatu na inatarajiwa kuendelea hadi mwisho wa wiki hii huku wanafunzi wakiendelea kutiririka kwa wingi.