Wakaazi wa eneo bunge la Bobasi ambao wana aina yoyote ya ulemavu wametakiwa kujitokeza kujiandikisha na idara ya kijamii ambayo inaendeleza shughuli hiyo kwa siku saba zijazo katika eneo hilo.
Haya yamesemwa na mshirikishi mkuu wa idara hiyo ya kijamii katika kaunti ya Kisii Bi Emmy Morage, aliyekuwa akiongea na mwandishi huyu siku ya Jumatatu, ambapo aliwahimiza wazazi pamoja na walezi kutowaficha watoto hao, bali wawelete kwenye vituo vilivyoteuliuwa mahusus kwa suala hilo.
'Tupo tayari kushirikiana na jamii ili kuhakikisha kwamba kila mtoto aliye na kasoro ya kimwili anaangaliwa vilivyo na kusiwe na aina yoyote na ubaguzi katika sehemu wanakosomea au katika makazi yao,” alisema Morage.
Bi Morage aliongeza kuwa usajili huo unalenga kusaidia kujua idadi ya watu wanaoishi na hali hiyo ili kuwa rahisi kwao kupata msaada wa kifedha unaopewa na serikali kuu, huku akisema kuwa wapo tayari kuwafaa watu wote walio na shida ya kimaumbile na ya kiakili, kufaulisha ndoto zao maishani.
Wakati huo huo, mkurugenzi mkuu wa idara hiyo katika kaunti ya Kisii Bwana Charles Rogito, ambaye alikuwa anaendeleza kampeni hiyo katika vituo mbali mbali aliwataka wazazi kuepukana na kuwabagua watoto hao na kuwataka walezi pia kuhusika katika kuwapeleka shuleni ili kuwaonyesha upendo.