Hali angavu na ya utulivu imerejea chuoni Maseno siku moja baada ya moto kuteketeza baadhi ya afisi za chuo hicho.

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Kufikia Ijumaa asubuhi, shughuli za biashara zilikuwa zimefunguliwa, baada ya kufungwa siku ya Alhamisi kupitia vurugu ya mkasa wa moto uliozua hali ya wasiwasi miongoni mwao. 

Wahudumu wa bodaboda pia nao walionekana asubuhi mapema wakiziendeleza shughuli zao za uchukuzi kama kawaida, ikilinganishwa hali yao chache baada ya mkasa huo wa Alhamisi usiku.

Akidhihirisha furaha yake, Mike Omondi, mmoja wa wahudumu wa bodaboda alimwambi mwandishi huyu wa habari kuwa mkasa huo uliadhiri biashara yao, kwani wengi wa wateja wao  ni wanafunzi na waadhiri wa chuo hicho.

“Wateja walikuwa wachache lakini leo ni wengi ilivyo desturi, mkasa huo ulikua umeathiri biashara lakini sasa hali iko sawa,” alisema Omondi. 

Wanafunzi pia walionekana wakiwa katika shughli zao kama ilivyo desturi, huku wengi wakielekea madarasani kama kawaida. 

“Nilikuwa na hofu kuwa tungefukuzwa kwenda nyumbani baada ya kisa cha moto, lakini tumeshukuru tuko shule na hali ni shwari,” alisema Faith Amolo, mwanafunzi chuoni.

Aidha, wafanyikazi wa chuoni humo walionekana wakiwasili kwa uchache, wengi wao wakiwa wamechanganyikiwa kwa kutojua pa kwenda ama cha kufanya kwani afisi zao zilikuwa zimeteketea. 

Moto huo uliteketeza mali ambayo uchunguzi bado unafanywa kubaini kiwango cha hasara. 

Polisi wanaendelea na uchunguzi ili kutathmini chanzo cha moto huo, na pia kumtia nguvuni yeyote aliyehusika katika kisa hicho.