Zaidi ya vijana 30 kutoka kaunti ya Mombasa walioathirika na utumizi wa dawa za kulevya wamekiri kuacha kutumia dawa hizo.
Vijana hao waliyopokelekwa na gavana wa kaunti ya Mombasa Hassan Ali Joho siku ya Ijumaa katika afisi ya gavana huyo mjini Mombasa wamesema kuwa wameamua kujinasua katika janga hilo baada ya kutumia dawa hizo kwa kipindi cha miaka zaidi ya tisa.
Vijana hao wameiomba serikali ya kaunti ya Mombasa kupokea na kuwapeleka katika vituo vya kurekebisha tabia ili kupokea matibabu yatakayowasaidia kubadilisha hali yao ya kiafya na wakaahidi kutorejea maskani wanakotumia dawa hizo.
“Wataomba gavana wetu Joho utusaidia tutoke katika janga hili la utumizi wa dawa za kulevya.Tumeathirika gavana sisi hata hatujui watoto wetu na wake zetu wako wapi.Tumewaibia wazazi wetu mali zao na kuuza ili tupate kununua unga,” alisema moja wa vijana hao.
Kwa upande wake gavana wa kaunti y hiyo Hassan Ali Joho ameahidi kuwapeleka vijana hao katika vituo vya kurekebisha tabia na akawaonya kutokwepa matibabu punde tu shughuli hiyo itakapoanza.
Gavana Joho akiwahimiza vijana wote waliyojitosa katika utumizi wa mihadarati kujitokeza na kupata matibabu. Aidha, ameahidi kutoa usaidizi kwa vijana watakajitokeza kupata matibabu kisha baadaye kupewa nafasi za ajiri ili kuzisaidia jamii zao.
“Wale wote watakaojitokeza ili kupata matibabu kwa kukubali kuacha kutumia dawa za kulevya basi watatibiwa kisha wapewa nafasi za ajira na kuwasadia jamii zao.Jukumu hilo sisi kama viongozi tuko tayari kuwasaidia vijana,” alisema gavana Joho.
Kwa sasa vijana hao wamepelekwa kwa shirika la kupambana na utumizi wa dawa za kulevya hapa pwani la Reachout Centre Trust ili kupata ushauri pamoja na kuanza zoezi la kupokea matibabu.